Maendeleo halisi ya kiuchumi nchini hayatapatikana hadi hapo rushwa kubwa itakapopigwa vita na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mwenyekiti mtendaji wa IPP Dr Reginald Mengi ametoa angalizo hilo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti ya umoja wa mataifa ya mwaka 2013 ya maendeleo ya kiuchumi, iliyozinduliwa nchini na mwenyekiti wa shirikisho la viwanda –CTI Bw. Felix Mosha.
Akizindua ripoti hiyo mbele ya wadau mbalimbali na wanachuo wa kituo cha kidiplomasia Tanzania , mwenyekiti wa CTI Bw. Felix Mosha amesema ripoti hiyo imebainisha mapungufu yanayokwamisha biashara baina ya nchi za Afrika na kupendekeza mbinu za kuendeleza biashara hizo ikiwemo kuimarisha na kuiwezesha sekta binafsi.
Akichangia hoja wakati wa uzinduzi huo mhadhiri mwandamizi wa chuo kikuu Dar es Salaam Prof. Lucian Msambichaka ametahadharisha kuwa Afrika, inayoongoza duniani kwa utajiri wa raslimali na kwa umaskini uliotopea, haitaweza kujikwamua kiuchumi kama haitawekeza vya kutosha katika raslimali watu.
Uzinduzi wa ripoti hiyo umeshuhudiwa pia na wadau mbalimbali akiwemo mkurugenzi mtendaji wa CTI Bibi Christine Kilindu, balozi mstaafu Ahmed Kiwanuka.