Utekelezaji kwa vitendo wa makubaliano yanayofikiwa wakati wa majadiliano baina ya sekta binafsi na serikali ndiyo yatakayoboresha mazingira ya uwekezaji nchini .
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi Tanzania – Tpsf bw. Godfrey Simbeye ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizindua ripoti mpya ya utafiti kuhusu hisia na maono ya viongozi wa biashara kuhusu ufanyaji biashara Tanzania, mbele ya wadau mbalimbali wa biashara nchini Utafiti huo mpya umebainisha kuwa tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika, uwingi na viwango vikubwa vya kodi na tozo, rushwa, udhaifu wa menejimenti ya kodi, na ugumu wa taasisi za fedha kukopesha wajasiriamali ni kikwazo vikuu vinavyokwamisha uwekezaji nchini.
Mapema akichangia hoja wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dr. Reginald Mengi amesema anakubali kuwa serikali ina utashi wa kisiasa katika kupambana na rushwa, lakini amesema kuna mapungufu katika kushughulikia rushwa kubwa, ambalo ndilo janga la taifa.
Wakichangia mjadala baadhi ya wadau waliopata fursa hiyo wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo wameelezea umuhimu wa kudumisha utaratibu wa majadiliano baina ya serikali na sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya uwekezaji